
Mabingwa wa soka tanzani bara Dar es salaam Young Africans wamepewa siku 14 kuanzia hii leo kuhakikisha wanawalipa waliokuwa wachezaji wa klabu hiyo msimu uliopita, nahodha Shadrack Nsajigwa pamoja na Stephen Mwasika wanaoidai klabu hiyo jumla ya sh. milioni 15.5.
Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya
Shirikisho la soka nchini TFF iliyokutana jana ambapo pamoja na mambo mengine ilisikiliza
madai ya wachezaji hao.
Fedha hizo ni ada ya usajili ambayo klabu hiyo ilikubaliana na
wachezaji hao wakati ikiwasainisha mikataba.
Yanga imeshawalipa sehemu ya fedha wachezaji hao wawilia mbao
walitemwa katika usajili wa msimu huu ambapo bado Nsajigwa anadai sh. milioni 9
wakati Mwasika anadai sh. milioni 6.5.
Wakati huo huo kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya
Shirikisho la soka nchini TFF imethibitisha usajili wa wachezaji 620 kati ya
624 wa timu za Ligi Daraja la Kwanza iliypangwa kuanza kuunguruma hapo kesho
katika viwanja tofauti.
Wachezaji wanne ambao usajili wao umezuiwa mpaka watakapokamilisha
taratibu ni Emmanuel Simwanza Namwando wa African Lyon, Godfrey Bonny Namumana
(Lipuli FC), na Enyinna Darlington na Chika Keneth Chukwu wote wa Mwadui FC ya
Shinyanga.
Darlington na Chukwu ambao wote ni Wanigeria wamezuiwa mpaka
watakapowasilisha vibali vya kufanya kazi nchini kutoka Idara ya Uhamiaji
wakati Namumana aliyekuwa akicheza nchini Nepal bado hajapata Hati ya Uhamisho
wa Kimataifa (ITC).
Nayo African Lyon imetakiwa kufikia muafaka na AYOSA Academy
ambayo Namwando anatoka juu ya usajili kabla ya kuanza kumtumia mchezaji huyo.
Klabu ambazo zimemaliza nafasi zote 30 usajili katika FDL ni
Friends Rangers FC ya Dar es Salaam, na Stand United FC ya Shinyanga wakati
iliyosajili wachezaji wachache zaidi ni Burkina Faso FC. Klabu hiyo ya Morogoro
imesajili wachezaji 19 tu.
Vilevile Kamati hiyo vilevile imethibitisha usajili wa wachezaji
wanane wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) waliosajiliwa katika hatua ya pili
ya usajili iliyoanza Agosti 14 hadi 30 mwaka huu.
Wachezaji hao ni Samir Ruhava na Amani Simba (Ashanti United),
Robert Machucha na Said Ndutu (Yanga U20), Ayoub Masoud na Abdallah Selemani
(Coastal Union U20), Ramadhan Kipalamoto (Simba U20) na Henry Joseph (Simba)
ambaye tayari Hati yake Uhamisho wa Kimataifa (ITC) imeshawasili.
0 comments:
Post a Comment