Na Shaban Kondo
Rais wa Shirikisho la soka nchini TFF, Leodegar Tenga ameishukuru
Kamati ya ligi kwa usimamizi mzuri tangu ilipokabidhi jukumu la kuisimamia ligi
kuu katika mzunguko wa pili msimu uliopita.
Raisi Tenga amesema TFF iliamua kuanzisha Kamati hiyo kwa lengo la
kutaka klabu zijisimamie zenyewe ili kuongeza ufanisi, jambo ambalo limeleta
mabadiliko na kuondoka matatizo katika kuwalipa waamuzi na makamisha
wanaosimamia michezo ya ligi kuu pamoja na ligi daraja la kwanza.
Katika hatua nyingine rais Tenga amesema kamati hiyo pia
imefanikiwa kutekeleza wajibu wa kudumisha utulivu na utawala bora na hivyo
kusababisha kasi ya makampuni kutaka kuwekeza katika ligi kuu kuendelea kupewa
nafasi kubwa.
Pia amesema kuanzia msimu ujao 2014/2015 klabu za Ligi Kuu
hazitaruhusiwa kusajili wachezaji hadi zitakapowasilisha TFF ripoti zao za
mapato na matumizi zilizokaguliwa (Audited accounts), hivyo klabu husika
zijiandae kwa ripoti hizo za Januari hadi Desemba 2013.
Wakati huo huo, Rais Tenga amesema bado suala la tiketi za
elektroniki linafanyiwa kazi na benki ya CRDB ambayo ndiyo iliyoshinda tenda
hiyo na liko katika hatua nzuri, kwani nia ya TFF na benki hiyo kuona kuwa
linaanza haraka iwezekanavyo.
0 comments:
Post a Comment